Mikopo ya Asilimia 10 Inabadilisha Maisha kwa Watu Wenye Mahitaji Maalum
Msikilize Mariam Siafu, mwanachama wa Kikundi cha Maza kutoka Tanga, akieleza jinsi mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na Halmashauri ulivyomuwezesha kuinua biashara yake, kujitegemea kiuchumi na kurejesha matumaini ya maisha bora.
Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa kila kundi katika jamii, ikiwemo watu wenye mahitaji maalum, linapata fursa sawa za kiuchumi na maendeleo.
#MikopoYaAsilimia10 #UwezeshajiWananchi #WatuWenyeMahitajiMaalum #Tamisemi ya wananchi
“Nilikuwa na ndoto, lakini mtaji ulikuwa changamoto… leo tunasimama kama mfano wa mafanikio kwa vijana.”
Msikilize Careen Safari Banigwa kutoka kikundi cha Empire Youth Group cha Kata ya Maweni, Halmashauri ya Jiji la Tanga, akielezea jinsi mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na Halmashauri ulivyobadilisha maisha yao baada ya kupatiwa mkopo wa shilingi milioni 50 na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa vijana. #Vijana #MkopoAsilimia10 #Tamisemi ya wananchi #MaendeleoYaVijana #Empowerment
LUSHOTO -TANGA Msikilize Mwenyekiti wa Kikundi cha Vijana cha Perfect Milk, Bw. David Nyiru kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, akielezea namna mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na Halmashauri ulivyosaidia kukuza uchumi wa kikundi na kufungua fursa mpya za ajira kwa vijana wa Lushoto.
KAMATI YA UHAKIKI MIKOPO KIBONDO YAKAGUA VIKUNDI VYA WANAWAKE, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU VINAVYOTARAJIA KUNUFAIKA NA MIKOPO
Kamati ya uhakiki mikopo Wilaya ya Kibondo imefanya ziara ya ufuatiliaji na uhakiki wa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vinavyotarajia kupatiwa mikopo katika robo ya tatu na ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026, kwa lengo la kujiridhisha na utekelezaji wa shughuli zao kabla ya kunufaika na mikopo hiyo.
Ziara hiyo imefanywa na Halmashauri kupitia kamati ya uhakiki mikopo kwa ajili ya kuhakiki, kukagua na kutathmini shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na vikundi hivyo ili kuhakikisha vina sifa za kupatiwa mikopo katika awamu hizo.
Akizungumza katika kikao cha majumuisho baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibondo, Bi. Upendo Marango, amesema lengo la ziara hiyo ni kuvitembelea vikundi hivyo na kujionea shughuli wanazozifanya ili kuhakikisha mikopo inayotolewa inaleta matokeo chanya kwa wanufaika pamoja na jamii kwa ujumla.
Aidha, Bi. Marango amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na Watendaji wa Kata kuendelea kuvisimamia vikundi hivyo kwa karibu kwa kuwatembelea mara kwa mara na kufuatilia maendeleo ya shughuli zao, hususan miradi waliyoainisha kuitekeleza baada ya kupatiwa mikopo hiyo.
Kwa upande mwingine, amewasisitiza Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kata kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu suala la marejesho ya mikopo, hasa kwa vikundi vinavyochelewa kurejesha fedha kwa muda mrefu, ili kubaini changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati.
KAMATI YA MBIO ZA MWENGE MKOA WA KATAVI YAFANYA ZIARA KUKAGUA MIRADI PENDEKEZWA TANGANYIKA DC
Wajumbe wa Kamati ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 Mkoa wa Katavi kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Mei 14, 2026 wamefanya ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopendekezwa kupitiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 wilayani Tanganyika.
Ziara hiyo imelenga kujionea hali ya utekelezaji wa miradi hiyo, ubora wake pamoja na kiwango cha utekelezaji ili kuhakikisha miradi yote inayopendekezwa inakidhi vigezo vya kupitiwa na Mwenge wa Uhuru utakaotarajiwa kufika Wilaya ya Tanganyika Septemba 26, 2026. Wajumbe wa kamati hiyo walitembelea na kukagua miradi mbalimbali ya kijamii na maendeleo inayotekelezwa katika maeneo tofauti ya halmashauri.
Aidha, wataalamu wa Halmashauri walipata nafasi ya kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo, ikiwemo hatua zilizofikiwa, manufaa kwa wananchi pamoja na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wake. Kamati hiyo pia ilitoa maelekezo ya maboresho katika baadhi ya maeneo ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa kuhamasisha utekelezaji wa miradi yenye tija kwa jamii, huku Wilaya ya Tanganyika ikiendelea kujipanga kuhakikisha miradi yote itakayopitiwa inaonesha thamani ya fedha na kuwanufaisha wananchi kikamilifu.
Kutana na Kikundi cha Vijana cha Zasmiba kutoka Halmashauri ya Jiji la Tanga, kilichoanzishwa mwaka 2018 kwa lengo la kuchakata taka za plastiki na kuzigeuza kuwa fursa ya ajira na maendeleo.
Kupitia mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na Halmashauri kutoka mapato ya ndani, kikundi hiki kimefanikiwa kuongeza mtaji, kupanua shughuli za uzalishaji na kujikwamua kiuchumi.
Leo, Zasmiba kinaendesha kiwanda cha kuchakata plastiki na kutoa ajira kwa vijana 20 wanaofanya kazi kama vibarua, hatua inayochangia kuongeza kipato na kuboresha maisha ya familia nyingi.
Msikilize Katibu wa Kikundi, Said Khalfan, akieleza namna mkopo huo ulivyobadilisha maisha yao na kuwawezesha kufikia mafanikio makubwa ya kiuchumi.
#MikopoYaAsilimia10 #VijanaNaMaendeleo #AjiraKwaVijana #TAMISEMI ya wananchi
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR- MUUUB) imetoa mafunzo kwa viongozi na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM – TAMISEMI) yaliyolenga kuwajengea uwezo katika eneo la usimamizi wa utendaji kazi, ufungamanifu wa Mipango ya Maendeleo ya Kitaifa, Mpango Mkakati wa TAMISEMI na Shughuli za kila siku za Watumishi wa Makao Makuu, Mikoa, Halmashauri na Wadau wote ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
#ikulumawasiliano #maelezo #utumishiwaumma #ofisiyawazirimkuu
WATUMISHI TAMISEMI WAJENGEWA UWEZO ENEO LA USIMAMIZI WA UTENDAJI KAZI ILI KUWAHUDUMIA WANANCHI
Na OWM - TAMISEMI, Dodoma
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR- MUUUB) imetoa mafunzo kwa viongozi na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM – TAMISEMI) yaliyolenga kuwajengea uwezo katika eneo la usimamizi wa utendaji kazi, ufungamanifu wa Mipango ya Maendeleo ya Kitaifa, Mpango Mkakati wa TAMISEMI na Shughuli za kila siku za Watumishi wa Makao Makuu, Mikoa, Halmashauri na Wadau wote ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mafunzo hayo yametolewa jijini Dodoma Mei 14, 2026 na Bw. Oswin Mkinga na Paulo Jorojick wa OR- MUUB ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Mheshimiwa Rais, kwa nyakati tofauti ametuagiza watumishi wa umma viongozi na wasio viongozi kuhakikisha tunawahudumia Watanzania, hivyo Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Juma Selemani Mkomi ametulekeza tuje kuwapa mafunzo yatakayowajengea uwezo kiutendaji ili kuongeza ufanisi na tija katika kuwahudumia wananchi," amesema Bw. Mkinga.
Akiendelea kutoa mafunzo hayo, Bw. Mkinga amesema kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 35 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Watumishi wa Serikali wanatekeleza majukumu ya Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo mafunzo hayo yamelenga kukuza utendaji kazi unaojali wananchi na maslahi ya taifa kwa jumla.
Aidha, Bw. Mkinga ameongeza kuwa baadhi ya watumishi wa umma katika taasisi zao wanafanya kazi ambazo hazina mchango katika utekelezaji wa malengo ya taasisi zao na taifa, hivyo Mfumo wa e-Utendaji (PEPMIS) unasaidia kubaini mipango isiyofungamana, isiyopimika na ambayo haijibu matarajio ya wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu OWM-TAMISEMI Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Bi. Emma Lyimo amesema mafunzo ya mfumo wa e-Utendaji (PEPMIS) ni muhimu katika kutimiza malengo ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, hivyo amewataka watumishi na viongozi waliohudhuria mafunzo hayo kuyazingatia kikamilifu na kwenda kutekeleza majukumu yao
UNICEF KUBORESHA SHULE MTANDAO NCHINI ILI KUWAWEZESHA WANAFUNZI KUJISOMEA WENYEWE
• Prof. Shemdoe aahidi kutoa ushirikiano kwa UNICEF
Na OWM - TAMISEMI, Dar es Salaam
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto Ulimwenguni (UNICEF), Bi. Elke Wisch amekutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe na kuahidi kuwa UNICEF itaanzisha na kuboresha shule mtandano (online public schools) ambazo zitawawezesha wanafunzi wa kitanzania kujisomea wenyewe.
Mwakilishi huyo Mkazi wa UNICEF Bi. Elke Wisch ametoa ahadi hiyo Mei 13, 2026 alipomtembelea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe katika ofisi yake iliyopo Magogoni jijini Dar es Salaam.
Bi. Wisch amemueleza Prof Shemdoe kuwa, UNICEF kwa kushirikiana na Serikali, imefanya utambuzi wa shule ambazo zimeunganishwa na mtandao na itaendelea kufanya kazi na Serikali kwa lengo la kuhakikisha shule zote zinaunganishwa na mtandao ili wanafunzi wa kitanzania wananufaike na mtandao kitaaluma.
Akizungumza ofisini kwake na Bi. Wisch, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe ameahidi kuwa, ofisi yake itaendelea kushirikiana na UNICEF ili kuwezesha kukamilika kwa mpango wa kuanzisha na kuboresha shule mtandano nchini ambazo zitaleta tija kwa wanafunzi katika ujifunzaji na kwa walimu katika ufundishaji.
Katika kutimiza azma ya kuboresha shule mtandao, Prof. Shemdoe ameahidi kuendeleza ushirikiano na wadau wa sekta ya elimu ili kuhakikisha madarasa ya kidigitali yanaongezeka, na kwamba atakuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa mifumo ya kidigitali pindi itakapokuwa tayari kwa matumizi ya walimu na wanafunzi.
Aidha, Prof. Shemdoe ameahidi kuwa TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya katika utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance), na kuongeza kuwa ofisi yake itahakikisha mifumo ya taarifa inasomana katika vituo vya afya na hospitali za wilaya.
Kikao kazi hicho cha Prof. Shemdoe na Bi. Elke Wisch, kimejadili maboresho katika sekta ya elimu, lishe, afya, ulinzi na usalama wa watoto, maji na usafi wa mazingira.