Wakulima katika Halmashauri za Chamwino, Kondoa, Chemba na Kongwa wamepatiwa elimu ya uzalishaji wa Alizeti kwa kutumia kanuni bora za kilimo kupitia mashamba darasa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija.
Mafunzo hayo yametolewa na wataalam wa Wizara ya Kilimo kupitia Mradi wa Kuwezesha Upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo Tanzania (TAISP) tarehe 11 hadi 14 Mei 2026, mkoani Dodoma ambapo pia wataalam kutoa walikagua maendeleo ya mashamba darasa yaliyoandaliwa na vikundi mbalimbali katika kata na vijiji vya Halmashauri hizo.
Ufuatiliaji huo ulilenga kuona namna wakulima wanavyoshiriki kwa vitendo katika mafunzo ya kilimo cha Alizeti kwa kutumia mbinu bora za kilimo. Jumla ya vikundi vya wakulima 32 vyenye jumla ya wakulima 729 kwenye Halmashauri zilizotembelewa vimenufaika na mafunzo ya kilimo cha Alizeti kwa kutumia kanuni bora za kilimo kupitia mashamba darasa yaliyoanzishwa.
Akizungumza kuhusu manufaa ya mashamba darasa, mkulima Bw. Idi Omary Nchongoli kutoka kijiji cha Kinyasi, kitongoji cha Kinyasi-Kati, Halmashauri ya Chemba amesema kuwa wakulima wamepata elimu zaidi kuhusu kilimo cha Alizeti kwa kutumia kanuni bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Wadau wanaotekeleza Mradi wa (TANRICE3) wamekutana katika kikao cha sita kujadili taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kutoka kwa wadau pamoja na Vyuo 6 vya Mafunzo ya Kilimo (MATI) vya Ilonga; Mtwara; Igurusi; Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Kilimanjaro (KATC); Tumbi; Ukiriguru pamoja na Shule ya Kilimo Zanzibar, kwa lengo la kuwezesha ushiriki wa kutosha katika kutekeleza mradi huo.
Kikao hicho kimefanyika tarehe 13 Mei 2026 mkoani Kilimanjaro, na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka Wizara ya Kilimo; Wakala wa Taifa wa Mbegu za Kilimo (ASA); Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC); Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI); Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI); Wakufunzi kutoka Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (MATI); Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar; Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar na wawakilishi kutoka Serikali za Mitaa.
Taarifa zimejikita katika maendeleo ya uzalishaji wa mbegu; zana za kilimo; usimamizi wa miradi ya umwagiliaji; jinsia; masoko; maendeleo ya utekelezaji wa Mfumo wa Taifa wa Tathmini ya Miundombinu ya Umwagiliaji (kwa kutumia mfumo mpya wa kidijiti utakaotumika kusimamia na kutunza kumbukumbu za taarifa za mafunzo ya kilimo cha mpunga nchini (NaRDA).
Mshauri Elekezi wa Mradi wa TANRICE3, Bw. Takanori Tomizuka ameipongeza Serikali kwa kutenga shilingi milioni 67 kwa ajili ya mafunzo ya wakulima wa mpunga, hatua inayoongeza upatikanaji wa elimu sahihi ya kilimo cha mpunga na kuongeza uzalishaji.
Pia ametoa pongezi kwa Vyuo vya Kilimo nchini kwa kuweka kipaumbele katika suala zima la mafunzo kwa wakulima.
Mradi wa TANRICE3 unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan ( JICA) kwa jumla ya Dola za Marekani 6,102,085. Mradi umejikita katika kukuza tasnia ya zao la mpunga nchini kwa kuwajengea uwezo wakulima kupitia mafunzo ambapo hadi sasa jumla ya wakulima 6116 (wanaume 3291 na wanawake 2825 ) wamenufaika na mafunzo hayo, hatua iliyoongeza uzalishaji wa kutoka tani 3.25 kwa hekta hadi kufikia tani 4.63 kwa hekta sawa na ongezeka la 40%.
WAJUMBE WA BODI YA WAKURUGENZI TCB WAFANYA ZIARA YA KIKAZI MKOANI KAGERA.
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Aurelia K. N. Kamuzora, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Bw. Primus Kimaryo, leo tarehe 14 Mei 2026 wamefanya ziara ya kikazi mkoani Kagera kwa lengo la kujionea maendeleo ya sekta ya kahawa, kuimarisha usimamizi wa shughuli za uzalishaji pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia na miche bora kwa wakulima wa kahawa nchini.
Katika ziara hiyo, wajumbe wa Bodi walitembelea Kiwanda kikubwa cha Kahawa cha AMIMZA ambapo walipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za uchakataji wa kahawa na hatua zinazochukuliwa katika kuongeza thamani ya zao hilo ili kuendelea kuinua ubora wa kahawa ya Tanzania na kuongeza ushindani wake katika soko la ndani na nje ya nchi.
Aidha, wajumbe wa Bodi walitembelea kitalu kikubwa cha uzalishaji wa miche bora ya kahawa kilichopo Kijiji cha Ruanga, Kata ya Ruanga, Wilaya ya Muleba, ambapo walijionea juhudi zinazofanywa kuhakikisha wakulima wanapata miche bora yenye tija kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa zao la kahawa nchini.
Ziara hiyo pia iliwafikisha wajumbe katika shamba kubwa la vijana la Mradi wa BBT Makongora, ambapo walipata nafasi ya kujionea shughuli zote za uzalishaji shambani hapo pamoja na namna vijana wanavyoshiriki kikamilifu katika kilimo cha kahawa kupitia mifumo ya kisasa ya uzalishaji. Kupitia mradi huo, TCB inaendelea kuhamasisha ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo ili kuongeza ajira, uzalishaji na mchango wa sekta ya kahawa katika uchumi wa Taifa.
Ziara hiyo imeendelea kutoa nafasi kwa wajumbe wa Bodi kusikiliza mafanikio na changamoto zinazowakabili wadau wa sekta ya kahawa mkoani Kagera, sambamba na kuimarisha mikakati ya maendeleo ya zao hilo kuanzia ngazi ya uzalishaji, uchakataji hadi upatikanaji wa masoko yenye tija.
Bodi ya Kahawa Tanzania inaendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha sekta ya kahawa inakuwa endelevu, yenye ushindani na inayochangia kikamilifu katika kuongeza kipato cha wakulima na kukuza uchumi wa Taifa.
@wizara_ya_kilimo
Mtaalamu wa Maabara kutoka Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Bw. Emmanuel Mwakatobe, akitoa mafunzo kuhusu umuhimu wa matumizi ya mbegu bora kwa wanafunzi wa Sokoine University of Agriculture (SUA), ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uelewa wa kitaalamu na kukuza sekta ya kilimo nchini.
UZALISHAJI WA ALIZETI IKUNGI, ITIGI, IRAMBA NA MKALAMA MKOA WA SINGIDA
Wakulima wa zao la Alizeti katika Halmashauri za Wilaya za Ikungi, Itigi, Iramba na Mkalama mkoani Singida wameendelea kunufaika na elimu ya kanuni bora za kilimo cha Alizeti kupitia mashamba darasa yaliyoanzishwa na Mradi wa Kuwezesha Upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo Tanzania (TAISP) unaotekelezwa na Wizara ya Kilimo.
Zoezi la ufuatiliaji wa mashamba darasa ya Alizeti limefanyika tarehe 12-13 Mei 2026 mkoani Singida katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida na Singida Manispaa kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanazingatia kanuni bora za kilimo na kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti.
Kwa mujibu wa taarifa za utekelezaji, jumla ya wakulima 807 wamenufaika na mafunzo hayo katika halmashauri za Itigi (278), Ikungi (192), Iramba (157) na Mkalama (180), kupitia mashamba darasa ya alizeti yaliyoanzishwa na TAISP.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambaye pia ni Afisa Kiungo wa TAISP, Bw. Bruno John Magazi, amesema Wizara ya Kilimo imewezesha upatikanaji wa pembejeo ikiwemo mbegu bora na mbolea za kupandia na kukuzia, hatua iliyowezesha wakulima kujifunza kwa vitendo kilimo cha kisasa chenye tija.
Kwa upande wa Afisa Kilimo wa Kata ya Dung’unyi (Ikungi), Bi. Ester Simon Bayda; Afisa Mazao wa Itigi, Bw. Christopher Wilboard Ghumpi; na Afisa Kilimo wa Kata ya Tumuli (Mkalama), Bi. Veronica Josia Bathlomeo, wameiomba Serikali kuendelea kuwezesha upatikanaji wa mbegu kwa bei nafuu, kuendeleza elimu ya kilimo na kuongeza idadi ya mashamba darasa ili kuwafikia wakulima wengi zaidi.
Kwa pamoja, wakulima akiwemo Bi. Pili Isingo Siuhi (Ikungi), Bi. Janet Emmanuel Kitinka (Itigi), pamoja na wakulima wa Iramba na Mkalama akiwemo Bw. Miraji Athuman Mtitu na Bi. Rehema Kyula Nonti, wamesema mashamba darasa yamewasaidia kuongeza uelewa wa kilimo bora cha Alizeti na kuwapa matumaini ya kupata mavuno mengi kupitia mbegu bora za AGUARA 6 na HYSUN 33.
Naye, Afisa Kiungo wa TAISP katika Halmashauri ya Iramba, Bi. Emakulatha Peter Sulle, ameeleza kuwa mashamba darasa yamekuwa yakiwajengea uwezo wa kulima kisasa na kuongeza kipato cha kaya.
Matukio katika picha, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) Bw. Samuel Mshote alipokuwa akieleza umuhimu wa TFC kama mdau wa Mkutano wa Wabunge Wanawake (WPC) wa Jukwaa la Maziwa Makuu (FP-ICGRL) utakofanyika Novemba 2026 jijini Dar es Salaam.
Kupitia fursa hii muhimu kwa TFC, Bw. Mshote ameeleza kuwa TFC inaunga mkono malengo ya mkutano huu hasa katika maeneo ya uwezeshaji wa kiuchumi, usalama wa chakula, maendeleo jumuishi, ushiriki wa wanawake na vijana, pamoja na ushirikiano wa kikanda. Kwa kuwa wanawake ni sehemu kubwa ya nguvu kazi katika sekta ya kilimo, upatikanaji wa mbolea bora unachangia moja kwa moja kuboresha maisha ya familia na jamii.
Kupitia shughuli za TFC za kuagiza, kuchanganya na kusambaza mbolea, TFC inalenga kuongeza uzalishaji wa kilimo, kuimarisha upatikanaji wa chakula, kusaidia wakulima wadogo hasa wanawake na vijana, pamoja na kuhamasisha kilimo endelevu na kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, TFC inaamini kuwa ushirikiano wa kikanda katika kilimo, biashara na maendeleo ya viwanda ni muhimu kwa amani na ustawi wa kiuchumi wa ukanda wa Maziwa Makuu. TFC iko tayari kuendelea kushirikiana na Mabunge, Washirika wa Maendeleo, Mashirika ya Wanawake na Sekta Binafsi katika kuendeleza mageuzi ya kilimo na usalama wa chakula.
Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) leo Mei 13, 2026 imeshiriki katika hafla ya kusaini Mkataba wa Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa kwanza wa Wabunge Wanawake (WPC) wa Jukwaa la Maziwa Makuu (FP-ICGLR) utakaofanyika mwezi Novemba 2026, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya utiaji saini wa Mkataba huo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb) ameshukuru Jukwaa hilo kwa kuiamini Tanzania, kuja kufanya mkutano huo muhimu unaolenga kuimarisha uongozi wa wanawake na kukuza ushirikiano wa kikanda.
Ameeleza kuwa nafasi hii ni muhimu kwa Tanzania kuonesha ukarimu, maendeleo ya kidemokrasia na dhamira ya kuendeleza ushirikiano wa kikanda, hivyo Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa mkutano huu na kuwapa ushirikiano mzuri katika kipindi chote cha maandalizi hadi kufanyika kwa mkutano.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Bw. Samuel Mshote ameeleza kuwa TFC kama Taasisi inayomilikiwa na Serikali chini ya Wizara ya Kilimo yenye jukumu la kusaidia uzalishaji wa kilimo na usalama wa chakula, inaendana na malengo mapana ya Mkutano wa Bunge la Wanawake, hususan katika maeneo Uwezeshaji wa kiuchumi, Usalama wa chakula, Maendeleo shirikishi, Ushiriki wa vijana na wanawake katika shughuli za kiuchumi, na Ushirikiano wa kikanda.
Mkutano huo wa Wanawake umepangwa kufanyika Novemba 2 hadi 5 mwaka huu jijini Dar es Salaam huku ukitarajiwa kukusanya wabunge wanawake kutoka nchi 12 wanachama wa (FP-ICGLR).
Picha mbalimbali zikionesha watumishi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) wakishiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea yaliyofanyika katika Viwanja vya John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma. Katika maadhimisho hayo, watumishi wa TPHPA walitoa elimu kwa wananchi waliotembelea mabanda ya maonesho kuhusu afya ya mimea, udhibiti wa visumbufu vya mazao na umuhimu wa kulinda mimea kwa ajili ya kuimarisha usalama wa chakula nchini, huku picha nyingine ni vikundi mbalimbali vya burudani vikiongeza shamrashamra za tukio hilo.
Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania imetoa tuzo ya pongezi kwa Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo kwa uongozi wake uliotukuka katika kusimamia na kuendeleza afya ya mimea nchini kwa ajili ya kuimarisha usalama wa chakula na lishe. Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea yaliyofanyika katika Viwanja vya John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.
Tuzo hiyo ilipokelewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde aliyemwakilisha Waziri wa Kilimo katika maadhimisho hayo. Wakizungumza katika hafla hiyo, viongozi wa TPHPA walisema mchango wa Mhe. Chongolo umeendelea kuimarisha huduma za afya ya mimea, kudhibiti visumbufu vya mazao na kuongeza uzalishaji wa chakula nchini, hatua inayochangia ustawi wa sekta ya kilimo na uchumi wa taifa.
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha afya ya mimea nchini kama sehemu ya kuhakikisha usalama wa chakula na lishe kwa wananchi. Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania itaendelea kuimarisha huduma za afya ya mimea ili kuongeza tija katika Sekta ya Kilimo na kufikia malengo ya Agenda 10/30 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050. Kauli hiyo aliitoa wakati akimwakilisha Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea yaliyofanyika jijini Dodoma tarehe 12 Mei 2026.
Katika hotuba yake, Mhe. Silinde alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuimarisha huduma za kidijiti nchini ambazo zimeendelea kusaidia maendeleo ya sekta mbalimbali ikiwemo kilimo. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi katika kulinda bayoanuai ya mimea ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na uzalishaji endelevu wa chakula na lishe bora kwa wananchi wote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania, Prof. Joseph Ndunguru amesema Tanzania imefikia kiwango cha utoshelevu wa chakula kwa asilimia 130 katika mwaka 2024/2025, huku uzalishaji wa chakula ukifikia tani 23,783,128. Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na jitihada mbalimbali za kudhibiti visumbufu vya mazao ikiwemo operesheni ya kudhibiti baa la panya katika mikoa 19, ambapo ekari 408,109 za mazao ziliokolewa na zaidi ya wakulima 66,511 kunufaika.
Prof. Ndunguru ameongeza kuwa mamlaka hiyo pia imefanikiwa kudhibiti zaidi ya ndege waharibifu milioni 231 aina ya kwelea kwelea waliokuwa wakivamia mashamba ya mpunga, mtama na uwele, hatua iliyookoa takribani tani 1,611,000 za mazao. Vilevile, katika kukabiliana na viwavijeshi, TPHPA ilifanya operesheni za udhibiti katika hekta 219,411 kwenye wilaya 49 nchini na kuokoa zaidi ya tani 529,347 za mazao ya mahindi na mtama. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ilikuwa “Ulinzi wa Bayoanuai ya Mimea kwa Usalama wa Chakula na Lishe.”